Riwaya ya Mmeza Fupa ni riwaya iliyoshinda an kupewa tuzo ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa mwaka 2017. Katika tangazo la ushindi wa riwaya hii jopo la majaji lilitoa sifa zifuatazo: Si mno mtu kukutana na riwaya ya Kiswahili ambayo mwandishi wake amejidhihirisha kuwa ni mbuji wa lugha fasaha na ya kisanii, inayotiririka kitabia kwa hiari yake, na bila ya kuonesha dalili zozote kwamba imelazimishwa. Wahusika wake wote wamebuniwa kwa ustadi, na kupewa kazi muwafaka za kuziwakilisha tanzu na matabaka mbalimbali ya jamii - pamoja na mikinzano na mazingira yao ya kihistoria, ya kisiasa,ya kisaikolojia, ya kitamaduni, ya kimjini au ya kijijini. Licha ya kwamba matukio ya riwaya hii yanatokea katika kisiwa cha kubuni, maswala yanayojadiliwa humu ni miongoni mwa yale maswala sugu yanayoendelea kulisumbua bara la Afrika kisiasa, kijamii na kiuchumi. Riwaya hii inatudhihirishia mandhari mapya ya utanzu huu wa Fasihi ya Kiswahili.
Uzito wa mivutano ya karne na migongano ya zama hubebwa migongoni mwa mwanadamu. Huchuana na wakati, katika kupapatuana na tsunami ya matendo ya mwanadamu. Ndivyo alivyoibuka Bi. Msiri kwenye joto la visasi, akaponea chupuchupu kumezwa na chatu-binadamu. Siku ya kuteketezwa kwa familia yake yeye alikuwa mtoni kufua. Aliporudi nyumbani alipokewa na simanzi nzito na rekecho la harufu ya damu. Hapo hapakumweka, huo ukawa mwanzo wa yeye kuwa mfungwa huru, akalimeza fupa ndani ya mapito ya karne mbili zilizompitia utosini. Kwa kuwa kwake mgubia chumvi nyingi chini ya jua, aliyajua mengi yaliyotiwa kapuni wakati ule. Akaweza kuja kuyasimulia wakati mwengine kwa vijana wengine aliowaamini.